Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye, Alhamis hii anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi rasmi wa Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira, Tanzania (Uwaridi).
Uzinduzi huo utafanyika kwenye ukumbi wa Nafasi Arts Space uliopo Mikocheni jijini Dar es Salaam karibu na ofisi za ITV/Radio One kuanzia saa sita mchana.
Taarifa kutoka kwa Katibu Mkuu wa Uwaridi, Ibrahim Gama zimedai kuwa kwenye uzinduzi huo pia wamealikwa waandishi wakongwe wa riwaya nchini akiwemo, Shafi Adam Shafi, aliyejipatia umaarufu kwa vitabu vyake kama Vuta N’kuvute na vingine.
Umoja huo ulianzishwa kwa madhumuni ya kutetea maslahi ya waandishi wa riwaya za Kiswahili ambao kwa miaka mingi kazi zao zimeshindwa kuwanufaisha. Pia Uwaridi itapigania kurudisha usomaji wa riwaya za Kiswahili nchini.