Septemba mosi mwaka huu kumepangwa kufanyika maandamano nchi nzima yaliyoandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) yenye lengo la kupinga wanachokiita ni Ukandamizwaji na Unyonywaji wa Demokrasia nchini wakiyabatiza kwa jina la (UKUTA) yaani Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania.
Marekani kupitia ubalozi wake hapa Tanzania, imewatahadharisha wananchi wake waishio hapa nchini kuhusu maandamano hayo, Tahadhari hiyo inawataka raia wote wa Marekani waishio hapa nchini kuepuka kujihusisha na maandamano hayo ikiwa ni pamoja na kuepuka kujichanganya na vikundi visivyo na tija, kwa kuhofia huenda pakatokea viashiria vya uvunjifu wa amani hali itakayohatarisha maisha ya raia hao.
Marekani imekuwa mfano wa kuigwa katika kuhakikisha usalama wa raia wake waliopo ndani na nje ya nchi hiyo. Tahadhari iliyotolewa kwa raia wa Marekani waishio Tanzania ni mwendelezo wa jitihada mbalimbali za Taifa hilo lenye nguvu Duniani.
Moja ya kumbukumbu nzuri ni namna ambavyo Marekani kupitia Ubalozi wake nchini Ufaransa ilivyoweza kuwakusanya raia wake waliokuwa jijini Paris Ufaransa kufuatia tishio la shambulio la kigaidi lililofanyika Novemba 14 mwaka jana kwenye Uwanja wa Stade de France ilipokuwa ikichezwa mechi ya kirafiki kati ya Ufaransa na Ujerumani.
Suala hili haliishii tu kwenye mambo ya kisiasa bali hata kwenye Tasnia ya burudani ambapo mapema mwezi huu msanii wa Marekani Robyn Rihanna Fenty maarufu Rihanna alilazimika kuahirisha onesho lake kwenye jiji la Nice Ufaransa baada ya Ubalozi wa Marekani kuwa na hofu na usalama.
Hii inawafanya raia wa Marekani kuwa na uhuru wa kufanya kazi zao Duniani kote wakiwa na uhakika wa usalama wa maisha yao na mali zao.
source; mtembezi.com